Company History

Historia na Asili ya ICU Ltd

Chama Kikuu cha Ushirika Igembensabo (ICU) Ltd kilianzishwa mwaka 1993 baada ya kilichokuwa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Tabora - TARECU (1984) Ltd kiliposhindwa kumudu kuendesha shughuli zake kikamilifu na kuamua kugawanyika kwa hiari na kuunda vyama vikuu viwili ambavyo ni Western Zone Tobacco Co-operative Union (WETCU) Ltd na Igembensabo Co-operative Union (ICU) Ltd. Hivyo, ICU Ltd kilisajiliwa tarehe 27 Aprili, 1993 kwa namba ya usajili 5484. ICU Ltd kiliundwa kwa madhumuni ya kuhudumia wakulima wa pamba na mazao mchanganyiko na kilirithi madeni yote yaliyokuwa yanahusu zao la pamba na mazao mchanganyiko yaliyokuwa TARECU Ltd. Makao Makuu ya ICU Ltd yapo tarafa ya Bukene Wilaya ya Nzega. Hadi kufikia Mwezi Disemba 2024, ICU Ltd kilikuwa na Vyama wanachama 96 kutoka katika Wilaya za Igunga na Nzega.

Madhumuni ya ICU Ltd

Dhumuni kuu la ICU Ltd ni kustawisha hali ya uchumi ya wanachama wake kwa kufanya mipango ya kuendeleza shughuli za kilimo, zinazoendeshwa na vyama wanachama kwa kufuata misingi na taratibu za vyama vya Ushirika kwa kufanya mambo yafuatayo:

  • Kutafuta soko la mazao ya Pamba na mazao mengine mchanganyiko kwa lengo la kuyauza kwa bei nzuri kwa faida ya wanachama wake.
  • Kusambaza na kuendeleza mifumo imara ya kilimo bora cha pamba na mazao mengine ya kilimo.
  • Kuanzisha na kuendeleza mifumo imara ya kilimo bora cha pamba na mazao mengine ya kilimo.
  • Kutoa elimu ya Ushirika kwa wanachama wake na kuwajengea uwezo watendaji ili kuleta ufanisi na kuimarisha uchumi wa chama.
  • Kuanzisha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa mbalimbali.
  • Kumiliki, kukodi na kustawisha ardhi, majengo na vifaa mbalimbali kwa ustawi wa chama.
  • Kukodi, kununua na kuendesha mitambo na maghala ili kuweza kutoa huduma inayohitajika kwa wanachama wake katika shughuli za kilimo.
  • Kutoa huduma za kitaalam kwa wanachama, huduma hizo ni pamoja na masuala ya uhasibu, biashara, masoko, kilimo.
  • Kufanya mambo mengine yaliyo halali na ambayo ni ya lazima katika kufanikisha utekelezaji wa madhumuni ya chama.